Link-.http://www.catholicdioceseofshy.or.tz/utolewaji-wa-daraja-takatifu-la-ushemasi-kwa-mafratel-6-wa-jimbo-katoliki-la-shinyanga-24-1-2019/

Askofu wa jimbo Katoliki Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu ametoa daraja Takatifu la Ushemasi kwa Mafrateri sita (6) wakati wa adhimisho la Misa Takatifu katika Sikukuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo Mtume Januari 25 mwaka huu 2019 katika Kanisa Kuu la Jimbo, “Mama Mwenye Huruma,” lililoko Ngokolo katika Manispaa ya Shinyanga.

Hii ni kwa mara ya pili jimbo Katoliki Shinyanga limepata Baraka ya kupata Mashemasi sita (6) kwa mkupuo tangu lianzishwe mwaka 1956, ambapo mnamo mwezi Desemba,1993 Marehemu Askofu Kastori Sekwa aliwapa daraja la Ushemasi mafrateri Anthony Mboje (kwa sasa Marehemu), Filemoni Machagija, Lwanga Misana, Kizito Nyanga, Paulo Shija na Sosthenesi Masese (Kwa sasa ni Marehemu) ambao pia walipewe ushemasi ndani ya Kanisa Kuu “Mama Mwenye Huruma” ambalo mwaka huu linatimiza miaka 25 tangu litabarukiwe.

Tukio hili lilovuta wakazi wengi wa manispaa ya Shinyanga na kupambwa kwa nderemo na fifijo limekuja wakati Mhashamu Askofu Liberatus Sangu na Mapadri wengine wane (4), kati ya waliopewa ushemasi mwezi Desemba mwaka 1993 wakiwa katika kuadhimisha mwaka wa Jubilei ya Fedha tangu wapate daraja Takatifu la Upadri miaka ishirini na mitano iliyopita.

Akitoa mahubiri mafupi wakati wa masifu ya jioni iliyotangulia adhimisho hio ,askofu Sangu aliyataja majukumu ya shemasi kuwa ni utumishi wa kuitangaza kweli ya Kristo na aliwataka kuipokea zawadi ya ushemasi kwa moyo wa utii na unyenyekevu; na kwamba, inawapasa wawe mitume wa upendo, huku wakiishi maisha ya sadaka kwa ajili ya Mungu na watu wengine.

Aidha mara baada ya kutoa daraja la ushemasi askofu Sangu aliwataka waamini kuendelea kuwaombea mashemasi hao iliwaweze kufikia daraja takatifu la upadri.

Mashemasi hao mapya ni Shemasi Martine Jilala toka Parokia ya Mipa, Shemasi Martine Emmanuel Masanja toka Parokia ya Mipa, Shemasi Peter Tungu toka Parokia ya Ng’wanhuzi, Shemasi Peter Lyuba toka Parokia ya Malampaka. Wengine ni Shemasi Richard Masunga toka Parokia ya Malili na Shemasi Gregory Samile toka Parokia ya Salawe.

Sherehe hizi zimehudhuriwa na mapadri, watawa wa kiume na kike, viongozi mbalimbali wa Vyama vya Siasa na Serikari na madhehebu ya dini pamoja na maelfu ya waamini kutoka parokia thethini na mbili (32) za jimbo la Shinyanga na hata kutoka majimbo ya jirani yakiwamo Jimbo Kuu la Mwanza na Kahama.

Wakati huo huo, askofu Sangu amezindua maadhimisho ya jubilee ya miaka 50 ya Utume wa walei kijimbo, pamoja na mfumo mpya wa kulitegemeza jimbo utakaoanza kutumika mwaka huu ambao unaelekeza kila mkristo Mkatoliki mbatizwa atapaswa kulitegemeza jimbo kwa kuchangia kiasi cha shilingi elfu mbili mwaka. Kupitia michango hiyo inatarajiwa kuwa jimbo la Shinyanga linalo kadiriwa kuwa na jumla ya waamini lakitano litaweza kukusanya kiasi cha zaidi ya shilingi Bilioni moja ambazo zitatumika katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya jimbo ikiwemo kuwategemeza makatekista. Viongozi walei kutoka kila parokia ya jimbo wakiongozwa na  mkurugenzi wa utume wa walei jimbo Padre Gerald Luhende walishiriki kuwasha mishumaa32 kadiri ya idadi ya parokia zote za jimbo hilo.

MWISHO.